Lugha Nyingine
Uongozi wa juu CPC wapanga kazi ya kuzuia mafuriko, utoaji misaada na ukarabati wa miundombinu baada ya maafa
BEIJING - Kamati ya Kudumu ya Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) imefanya mkutano Alhamisi ulioongozwa na Xi Jinping, Katibu Mkuu wa Kamati Kuu ya CPC ili kujadili na kupanga kazi juu ya kuzuia mafuriko na kutoa misaada kwa waathirika, vilevile kurejesha hali ya kawaida na kufanya ukarabati wa miundombinu baada ya maafa.
Mkutano huo umebainisha kuwa China imepata mafanikio makubwa katika kuzuia mafuriko na utoaji misaada ya maafa.
Kwa vile China bado iko katika msimu mkuu wa mafuriko kwa sasa, dhoruba, mafuriko, vimbunga na majanga mengine bado yanatokea mara kwa mara katika maeneo mengi nchini humu, mkutano huo umesema.
Umeeleza kuwa juhudi hazipaswi kupunguzwa kwani hatari za mafuriko katika baadhi ya mabonde ya mito bado zipo na hatari ya mafuriko ya maji kutoka milimani katika sehemu za kaskazini na kaskazini mashariki mwa China ni kubwa, wakati hali ya ukame imetokea katika baadhi ya mikoa na haipaswi kuchukuliwa kuwa ni tatizo dogo.
Mkutano huo umezitaka serikali na idara husika za mitaa kila wakati kuweka kipaumbele kwa usalama wa maisha na mali za watu, na kuendelea kufanya vizuri kazi za kuzuia mafuriko na kutoa misaada kwa waathirika wa maafa.
“Jitihada zaidi zinapaswa kufanywa ili kuweka tahadhari ya wakati halisi ya mapema na kukabiliana na majanga, kuweka kipaumbele cha juu cha kuzuia mafuriko katika mabonde ya mito, na kuboresha na kutekeleza hatua za kuzuia na za kiusalama zinazohusiana na mafuriko katika mito midogo na ya kati na maeneo mengine dhaifu” mkutano umesema.
Mkutano huo umesisitiza kufanya juhudi za dharura za pande zote za uokoaji na utoaji msaada ili kuwasaidia watu waliokumbwa na maafa na kuwatafuta waliopotea ili kupunguza athari kwa maisha ya watu. Pia umehimiza juhudi za kuimarisha mabwawa ambayo ni muhimu au dhaifu, na kukidhi mahitaji ya kimsingi ya wakazi waliokumbwa na mafuriko ikiwa ni pamoja na kutumia fedha kwa kupata ufanisi katika kukarabati miundombinu iliyoharibika kama vile usafiri, mawasiliano na umeme, na kurejesha hali ya kawaida kwenye mashamba na vifaa vya kilimo.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma