Lugha Nyingine
Kenya yawa mwenyeji wa mkutano wa pamoja wa taasisi za Confucius barani Afrika
Wanafunzi wakitumbuiza kwenye mkutano wa pamoja wa taasisi za Confucius barani Afrika katika Chuo Kikuu cha Nairobi, Kenya, Mei 30, 2024. (Xinhua/Wang Guansen)
NAIROBI - Mkutano wa Pamoja wa Mwaka 2024 wa Taasisi za Confucius barani Afrika ulioandaliwa kwa pamoja na Mfuko wa Kimataifa wa China wa Elimu ya Lugha ya Kichina, Chuo Kikuu cha Nairobi, ambacho ni chuo kikuu kikongwe zaidi nchini Kenya, na Taasisi yake ya Confucius umeanza siku ya Alhamisi mjini Nairobi, Kenya, ili kujadili ushirikiano na maendeleo ya vituo vya mafunzo ya lugha ya Kichina katika bara zima.
Mkutano huo utakaoendelea hadi Juni 1, wenye kaulimbiu ya "Kuboresha Maendeleo, utaratibu na Ubunifu wa Taasisi za Confucius barani Afrika," unakutanisha wawakilishi zaidi ya 100 kutoka Taasisi za Confucius na Madarasa 77 ya Confucius barani Afrika.
Maofisa waandamizi wa serikali, wanadiplomasia, wanataaluma wa vitivo na wanafunzi walihudhuria hafla ya ufunguzi iliyofanyika katika Chuo Kikuu cha Nairobi.
Hafla hiyo ilijumuisha uzinduzi wa Muungano wa Taasisi ya Confucius wa Afrika Mashariki na Umoja wa Wahitimu wa Tianjin nchini Kenya.
Aurelia Chepkirui Rono, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nchi inayoshughulikia Masuala ya Bunge ndani ya Ofisi ya Waziri Mkuu wa Kenya, amesema "mkutano huu unaashiria hatua muhimu katika safari yetu ya pamoja ya kuendeleza ushirikiano wa karibu na kuchangiana mbinu bora katika ufundishaji wa lugha na utamaduni wa Kichina."
Amesisitiza mchango muhimu wa Taasisi za Confucius katika kukuza maelewano na kuimarisha uhusiano kati ya China na Afrika katika zama za kuongezeka kwa utandawazi wa dunia.
Rono amesifu historia yenye mambo mengi na mfumo wenye umaalum wa maendeleo ya China kama chanzo kikubwa cha hamasa kwa Afrika na kupongeza Taasisi za Confucius kwa kuwezesha mawasiliano kati ya watu na kuendeleza utalii wa kitamaduni.
Stephen Kiama, makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Nairobi, amesema kuwa mkutano huo unathibitisha dhamira ya Afrika na China kuondokana na vikwazo vya kitamaduni na lugha na kuendeleza mawasiliano kati ya pande zote.
Kwa mujibu wa Kiama, Taasisi za Confucius za barani Afrika zimekuwa vituo bora katika kuendeleza shughuli za kitamaduni za kuvuka mipaka, muhimu kwa kujenga Dunia ya kuheshimiana na yenye ustawi wa pamoja.?
Wanafunzi wakitumbuiza kwenye mkutano wa pamoja wa taasisi za Confucius barani Afrika katika Chuo Kikuu cha Nairobi, Kenya, Mei 30, 2024. (Xinhua/Wang Guansen)
Wanafunzi wakitumbuiza kwenye mkutano wa pamoja wa taasisi za Confucius barani Afrika katika Chuo Kikuu cha Nairobi, Kenya, Mei 30, 2024. (Xinhua/Wang Guansen)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma