Lugha Nyingine
Rais Xi Jinping akutana na mwenzake wa Tanzania Samia Suluhu Hassan
Rais Xi Jinping wa China akikutana na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ambaye yuko Beijing kwa ajili ya kuhudhuria Mkutano wa Kilele wa 2024 wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC), kwenye Jumba la Mikutano ya Umma mjini Beijing, China, Septemba 4 2024. (Xinhua/Li Tao)
BEIJING - Rais wa China Xi Jinping amekutana na Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan siku ya Jumatano, ambaye yuko Beijing kwa ajili ya kuhudhuria Mkutano wa Kilele wa 2024 wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) ambapo amesema mwaka huu ni maadhimisho ya miaka 60 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na Tanzania.
Kwenye mkutano huo, Rais Xi amesema China ingependa kuzidisha uhusiano wa kiwenzi na ushirikiano wa kimkakati wa pande zote kati yake na Tanzania ili kuleta manufaa zaidi kwa watu wa pande zote mbili na kuenzi urafiki wa jadi kizazi hadi kizazi.
China pia inapenda kutumia mkutano huo kama fursa ya kusukuma mbele maendeleo mapya katika mradi wa ufufukaji wa Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA), na kuboresha kwa pamoja mtandao wa usafiri wa reli na baharini wa Afrika Mashariki, Rais Xi amesema.
“Jitihada hizi zitasaidia Tanzania kuwa eneo la kielelezo la kuzidisha ushirikiano wa kiwango cha juu wa Ukanda Mmoja, Njia Moja kati ya China na nchi za Afrika” Rais Xi ameongeza.
Amesisitiza kuwa Tanzania ndipo mahali ambapo China ilipopendekezea kwa mara ya kwanza sera yake kwa Afrika kwa zama mpya.
Akirejelea Makubaliano ya Dar es Salaam kati ya China na Afrika yaliyotolewa kwa pamoja na wasomi wa China na Afrika nchini Tanzania mwezi Machi, Rais Xi amesema yanaonyesha makubaliano kati ya nchi za Kusini kuhusu njia na falsafa ya maendeleo.
Uhusiano kati ya China na Tanzania unaendana na mwelekeo wa kihistoria wa maendeleo ya Nchi za Kusini, ukishikilia maadili muhimu na kubeba jukumu kubwa, Rais Xi amesema.
Kwa upande wake Rais Samia amesema anaamini kwamba mkutano wa kilele wa FOCAC mjini Beijing utatoa mchango mpya katika kuzidisha ushirikiano wa kirafiki kati ya Afrika na China na kuendeleza kwa kiasi kikubwa maendeleo ya viwanda na mambo ya kisasa ya kilimo barani Afrika.
Huku akiongeza kuwa China ni mwenzi wa kutegemewa na asiyekosekana wa Tanzania, Rais Samia amesema nchi yake ingependa kushirikiana kikamilifu na China kuendeleza ushirikiano wa Ukanda Mmoja, Njia Moja.
Rais Xi Jinping wa China akikutana na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ambaye yuko Beijing kwa ajili ya kuhudhuria Mkutano wa Kilele wa 2024 wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC), kwenye Jumba la Mikutano ya Umma mjini Beijing, China, Septemba 4 2024. (Xinhua/Yin Bogu)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma