Lugha Nyingine
Waziri wa Mambo ya Nje wa China atoa wito wa juhudi za pamoja za kuendeleza mazungumzo ya amani juu ya Ukraine
Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi, ambaye pia ni Mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), akihudhuria mkutano wa ngazi ya juu wa Baraza la Usalama kuhusu hali ya Ukraine kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa huko New York, Septemba 24, 2024. (Xinhua/Xie E)
UMOJA WA MATAIFA - Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi wakati akihudhuria mkutano wa ngazi ya juu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya Ukraine uliofanyika kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa huko New York siku ya Jumanne, amesema kuwa pande zote zinapaswa kuwa na dhamira ya kweli katika kuendeleza mazungumzo ya amani juu ya suala la Ukraine.
“Baraza la Usalama linapaswa kuwa daraja kati ya tofauti na mikanganyiko, mtetezi wa kutafuta maelewano ya pamoja huku likiondoa tofauti, mlindaji wa usalama wa pamoja, na mjenzi wa amani ya kudumu,” amesema Wang, ambaye pia ni Mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC).
Wang ametoa mapendekezo matatu kuhusu suala hili:
Kwanza, ni muhimu kuongeza uelewa kuhusu msukosuko katika hali ya kutuliza mgogoro. Silaha za maangamizi makubwa hazipaswi kutumiwa, vifaa vya nyuklia vilivyowekwa kwa malengo ya amani kama vile vinu vya nyuklia havipaswi kushambuliwa, na raia na vifaa vya kiraia havipaswi kulengwa.
Pili, ni muhimu kuongeza uelewa juu ya uwajibikaji katika kuhimiza mazungumzo ya amani. Mazungumzo na majadiliano ni njia pekee ya kumaliza mgogoro wa Ukraine, na jumuiya ya kimataifa inapaswa kutumia fursa iliyopo sasa kuanzisha juhudi za pamoja za kuhimiza mazungumzo ya amani.
Tatu, ni muhimu kuongeza uelewa kuhusu hali ya dharura katika kudhibiti kupanuka kwa mgogoro. China inatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuimarisha ushirikiano katika masuala ya nishati, fedha, biashara, usalama wa chakula na ulinzi wa miundombinu muhimu kama mabomba ya mafuta na gesi, ili kudumisha kwa pamoja utulivu na mzunguko mzuri wa minyororo ya viwanda na usambazaji wa bidhaa duniani.
Mwanadiplomasia huyo mkuu wa China amesema, China si muanzishaji wa mgogoro wa Ukraine, wala si upande unaohusika na mgogoro huo. China siku zote imekuwa ikiunga mkono amani, na kudumisha mawasiliano na pande zote, zikiwemo Russia na Ukraine, ameongeza.
Huku akionya kwamba jaribio lolote la kulaumu, kushambulia au kuipaka matope China kuhusu suala la Ukraine ni kutowajibika na halitafanikiwa, Wang ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kushikana mikono na kufuata maono ya usalama wa pamoja, jumuishi, wa ushirikiano na endelevu.?
Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi, ambaye pia ni Mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), akihudhuria mkutano wa ngazi ya juu wa Baraza la Usalama kuhusu hali ya Ukraine kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa huko New York, Septemba 24, 2024. (Xinhua/Li Rui)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma