Lugha Nyingine
Rais wa Uganda asema yuko tayari kusuluhisha mgogoro wa Sudan
Rais wa Uganda Yoweri Museveni amesema yuko tayari kuwa mpatanishi wa amani katika mgogoro unaoendelea nchini Sudan ambao umesababisha vifo vya maelfu ya watu na mamilioni ya wengine kukimbia makazi yao.
Rais Museveni amesema hayo wakati alipokutana na Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia suala la Sudan, Ramtane Lamamra.
Rais Museveni ameongeza kuwa yuko tayari kusuluhisha mgogoro huo kama watakubali, na kuzitaka pande zinazopigana kukubaliana kusimamisha mapigano na kukabidhi madaraka kwa watu wa Sudan.
Kwa upande wake Lamamra amemhakikishia Museveni kwamba Umoja wa Mataifa utamuunga mkono kutatua mgogoro huo.
Wakati huohuo Mtandao wa Madaktari wa Sudan usio wa kiserikali jana ulitangaza kuwa takriban watu 20 wameuawa na wengine watatu kujeruhiwa katika shambulizi lililofanywa na Wanajeshi wa Kikosi cha Mwitikio wa Haraka (RSF) katika kijiji kimoja cha Jimbo la Kordofan Kaskazini Magharibi mwa Sudan. Mtandao huo haukutoa maelezo ya ziada, na RSF bado haijatoa maoni yoyote kuhusu shambulizi hilo.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma