Lugha Nyingine
Jumba la makumbusho linaloonyesha ustaarabu wa China wa miaka 4,000 iliyopita lafunguliwa
Kitu kinachooneshwa kwenye Jumba la Makumbusho ya mabaki ya kale ya Taosi katika Wilaya ya Xiangfen, Mkoa wa Shanxi, Kaskazini mwa China, Novemba 12, 2024. (Xinhua/Yang Chenguang) |
TAIYUAN - Jumba la Makumbusho ya mabaki ya kale ya Taosi linaloonyesha mabaki ya kitamaduni yenye historia ya kuanzia miaka 3,900 hadi 4,300 iliyopita limefunguliwa kwa umma jana Jumanne katika Mkoa wa Shanxi, Kaskazini mwa China, likionyesha hali ya kuundwa kwa dola ya mwanzo ya China na utatanishi wa kijamii.
Jumba hilo lililo katika Wilaya ya Xiangfen ya mkoa huo limejengwa kwenye ukingo wa kaskazini-magharibi wa eneo la mabaki kitamaduni ya Taosi kufuatia miaka 46 ya kazi ya kiakiolojia.
Eneo la mabaki ya kitamaduni la Taosi linaaminika kuwa na uwezekano mkubwa wa kuwa magofu ya mji mkuu wakati wa enzi za Yao na Shun -- wafalme wawili wenye hekima katika miaka zaidi ya 4,100 iliyopita.
Watembeleaji wa jumba hilo wanaweza kuchangamana na meza inayoonesha mfano wa miundombinu ya enzi hizo ili kutazama ramani ya mji wenye ukubwa wa mita za mraba zaidi ya milioni 2.8.
Katika mji huo wa kale, matokeo ya utafiti yanaonyesha kwamba watu wa Taosi walilima mtama, kufuga mifugo, na kuendeleza ufundi wa kazi za mikono kama vile vyombo vya udongo, vyombo vya jade, na vyombo vya lacquer, vikitengeneza utamaduni mzuri wa mijini.
Magofu ya mji huo yanajumuisha misingi ya majengo ya kasri yenye ukubwa wa mita za mraba 6,500, ambayo ni muundo mkubwa zaidi wa ardhi ya moramu wa nyakati za kabla ya historia kuwahi kupatikana, amesema Gao Jiangtao, kiongozi wa timu ya wanaakiolojia ya Taosi chini ya Taasisi ya utafiti wa Akiolojia ya Akademia ya Sayansi ya Jamii ya China.
"Matokeo haya yanaonyesha awamu mpya muhimu katika uundaji na maendeleo ya ustaarabu wa China," Yan Yalin, mkurugenzi wa idara ya akiolojia ya Mamlaka ya Urithi wa Kitaifa wa Utamaduni ya China.
Wataalamu wamesema kwamba Taosi huakisi sifa za awali za jamii ya nchi ya China, ikionyesha mienendo ya enzi za kiutawala zilizofuata baadaye.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma